watu walio tembelea leo

Wema: Sitarudi nyuma vita ya ubunge.


Licha ya kukumbana na maoni na mitazamo tofauti kufuatia kutangaza nia yake ya kugombea ubunge, Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, amesema hatakata tamaa wala kurudi nyuma katika dhamira yake ya kuingia katika siasa.
 
Juzi asubuhi Wema aliandika tena katika ukurasa wake wa Instagram kwamba yuko tayari kukabiliana na changamoto za aina zote katika safari yake ya kuelekea bungeni.
 
"Nimethubutu na sitarudi nyuma, niko tayari kwa mashambulizi ya aina yoyote," aliandika kwa kifupi mrembo huyo ambaye safari yake ya Miss Tanzania ilianzia katika kitongoji cha Dar Indian Ocean na baadaye Kanda ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
 
Mrembo huyo alikisifu pia Chama Cha Mapinduzi na kuwataka wanawake wengine wasihofie kushiriki katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi pale wanapoona muda wao umefika.
 
Juzi, Wema aliandika kwenye ukurasa wake huo kwamba atawania ubunge wa viti maalum kupitia CCM mkoa wa Singida katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
 
Wema ambaye alifuatana na mama yake mzazi, Mariam Sepetu, aliweka hadharani dhamira yake hiyo walipokuwa mkoani Singida mbele ya viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa.
 
Alisema kuwa anatarajia kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ya ubunge Julai 15, mwaka huu huku akiongeza kwamba maamuzi yake ya kuingia kwenye ulingo wa siasa yalikuwa kwenye moyo wake na alishawahi kumueleza marehemu baba yake (Balozi - Isack Sepetu) ambaye alimwambia kwamba anaweza na muda ukifika asiache kujihusisha.
 
Aliongeza kwamba katika harakati hizo hatakubali kuona anashindwa ingawa anafahamu wazi kuwa atakutana na changamoto mbalimbali baada ya kuanza kwa mchakato huo.
 
Alisema kwamba licha ya kusoma masomo yanayohusu Biashara ya Kimataifa badala ya siasa, marehemu baba yake hakukata tamaa na alimtaka ajihusishe na masuala ya siasa.
 
Mrembo huyo ambaye pia ni msanii wa filamu za Kitanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Endless Fame ambayo kazi yake ni kuibua wasanii na kuwasimamia kwenye tasnia hiyo, anaamini kwenye nia hakuna kinachoshindikana.