
Msanii Juma Nature.
Dar es Salaam. Msanii Juma Nature, ametoa rai kwa wasanii waliotangaza nia kuwania viti mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao, akiwataka kusimama kwenye misingi ya kusaidia jamii badala na si vinginevyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Nature ambaye
mapema mwaka huu alifuta msimamo wake wa kutaka kugombea ubunge Jimbo la
Temeke alioutangaza miaka mitatu iliyopita, alisema kwamba ni vyema
wasanii wanaosaka nafasi za kisiasa kuzingatia watakayotakiwa kufanya
kwa mujibu wa nafasi hizo za uwakilishi.
Nature alisema ni muhimu kufuata matakwa ya
wananchi watakaowaongoza na kuacha kuweka mbele tamaa ya fedha kwa kuwa
hayo siyo malengo ya uongozi wa kijamii bali huduma kwa wananchi.
“Kama wanaingia kwa ajili ya kwenda kwenye ubunge
ni sawa, kwani wao ni watunzi wazuri wa zamani na uandishi wao upo
kwenye jamii, lakini wasiende wakifikiria uongozi kuwa sehemu ya
kujipatia fedha. Wawe karibu na wananchi watakaowaongoza kwa sababu hiyo
ndiyo iliyo chini yao na inawategemea,” alisema Nature.
Kwa mujibu wa Nature ameamua kukaa pembeni kwa
muda kutokana na utitiri wa wasanii walioweka wazi dhamira zao za
kujiingiza katika siasa mwaka huu.
Alisema wazo hilo alilokuwa nalo muda mrefu,
ameamua kujipa muda hadi ifikapo mwaka 2020 ili kuwaacha waliotangaza
nia sasa kuendeleza mchakato huo.
“Mwenyezi Mungu akipenda ni tagombea mwaka 2020,
nimeamua kwa mwaka huu niache mambo haya kwanza. Sasa nina kazi nyingi.
Pili wasanii wengi wameshajitokeza, inatosha sana. Tusubiri tuone kwamba
watafanya nini, ndipo na sisi tutaona nini tunafanya,” alisema Nature
akiongeza kuwa kwa sasa yupo katika matengenezo ya video ya “Inaniuma
Sana Remix” aliyomshirikisha Msaga Sumu.